Wafanyakazi wa IOM wanatarajiwa kuwa na viwango vya juu vya tabia za kibinafsi na kiwango cha juu zaidi cha uadilifu. Tabia za wafanyakazi wa IOM – hata wasipokuwa kazini na hata kama hazihusiani na majukumu – hazipaswi kutia hatarini maslahi ya IOM, kuiletea kashfa au kuudhi jamii ambamo wanafanya kazi. Wafanyakazi wa IOM wanatarajiwa kuweka manufaa ya Shirika mbele ya maslahi ya kibinafsi, kitaifa au mengine.

Maadili ya Msingi ya IOM

Watu wote walioajiriwa au wanaofanyia IOM kazi duniani kote wanastahili kufuata Viwango vya Maadili vya IOM. Maadili ya Msingi ya IOM yanajumuisha:

  • Uaminifu
  • Uadilifu
  • Uhuru
  • Kutopendelea
  • Mtazamo wa kimataifa
  • Uhuru wa kutobaguliwa
  • Uhuru wa kutodhalilishwa
  • Usawa wa kijinsia
Mifano ya Hali Zinazohitaji Tahadhari

Kuna hali nyingi ambapo wafanyakazi wa IOM wanapaswa kuwa waangalifu au kuomba ushauri zaidi.

Kwa mfano:

  • Mgongano wa maslahi
  • Matumizi ya mali na rasilimali za IOM
  • Mahusiano na serikali
  • Mahusiano na umma
  • Mawasiliano na vyombo vya habari
  • Matumizi na ulinzi wa taarifa, ikiwa ni pamoja na kwenye mitandao ya kijamii
  • Kuheshimu tamaduni na desturi za wenyeji
  • Tabia za kibinafsi
  • Ajira na shughuli za nje
  • Shughuli za kisiasa
  • Zawadi, heshima na ujira kutoka nje.

Wafanyakazi wa IOM ambao wana maswali kuhusu maadili katika shirika la IOM wanapaswa kupitia upya Viwango vya Maadili ya IOM au wawasiliane na Ofisi ya Maadili na Mienendo katika ECO@iom.int.

Mifano ya aina zingine za mienendo mibaya katika shirika la IOM iliyosababisha hatua za kinidhamu kuchukuliwa
  • Mfanyakazi alionekana kwenye vyombo vya habari kwa njia ambayo iliashiria mfungamano wa kisiasa wenye utata.
  • Mfanyakazi alimshambulia dereva akiwa kazini katika jamii ambayo IOM inaendesha shughuli zake.
  • Mfanyakazi alitenda visivyo akiwa hayuko kazini na alifanya uamuzi mbaya uliosababisha kukamatwa kwake na polisi wa eneo hilo.
  • Mfanyakazi alitumia “Facebook” kuchapisha maoni yasiyofaa kumhusu mwanasiasa na familia yake.
  • Mfanyakazi alitembelewa ofisini mwake wakati wa kazi na mgeni kutoka nje ambapo walishiriki vitendo vya kimapenzi ambavyo havikufaa mbele ya wafanyakazi wenzake.
  • Mfanyakazi aliripoti kazini akiwa mlevi na akabishana na mgeni kutoka nje.
  • Mfanyakazi alishiriki katika shughuli za nje zisizojulikana, akitoa huduma zile zile zinazotolewa na Shirika.
  • Mfanyakazi alikosa kufika kazini mara kadha wa kadha bila ruhusa.
  • Mfanyakazi alitoa taarifa zisizo za kweli, zisizowiana na za kupotosha kwa Ofisi ya Uangalizi wa Ndani (OIO) wakati wa uchunguzi.
  • Mfanyakazi alikaidi wakuu wake na kuwasiliana isivyofaa na wawakilishi wa Serikali.
  • Wafanyakazi walikosa kuripoti mara moja shughuli haramu za mawakala wa nje katika majengo ya IOM.
  • Mfanyakazi alikiuka sheria ya kitaifa na kushindwa kufuata maagizo yaliyotolewa kabla ya safari rasmi.
  • Mfanyakazi alitoa jina lao la mtumiaji na nenosiri ili kumwezesha mfanyakazi mwingine wa IOM kuidhinisha hati anuwai za kifedha na kiutawala ambazo ni yeye tu aliyekasimiwa mamlaka na jukumu la kuidhinisha.
  • Mfanyakazi alishiriki katika ukatili wa nyumbani.

 

Wafanyakazi wa IOM huwakilisha Shirika wakiwa kazini na vilevile wakati wao wa mapumziko na sharti wafanye kila wawezalo ili kulinda uadilifu na sifa za IOM na waepuke mienendo mibaya. Wafanyakazi wa IOM wana wajibu wa kuripoti mienendo mibaya. Wafanyakazi wa IOM wanaoripoti kwa nia njema wana haki ya kulindwa dhidi ya ulipizaji kisasi (tazama https://weareallin.iom.int/sw/ulipizaji-kisasi).

 

Inaweza kuwa vigumu kutofautisha aina mbalimbali za mwenendo mbaya. Huhitaji kujua aina ya mwenendo mbaya ili uweze kuripoti. Iwapo utapata au kushuhudia mwenendo mbaya wowote, makosa au ikiwa unahisi kuwa kuna kosa lililofanyika, unapaswa kuripoti kwa Ofisi ya Uangalizi wa Ndani (OIO) ya IOM kupitia jukwaa la kuripoti mwenendo mbaya la IOM, “We Are All In” (www.weareallin.iom.int) au kwa baruapepe kwa oiointake@iom.int, hata kama huna hakika hiyo ni aina gani ya mwenendo mbaya.


Ilisasishwa mwisho: Machi 2024