IOM imejitolea kuwalinda wafanyakazi wa IOM wanaoripoti mienendo mibaya, au wanaoshirikiana na ukaguzi na uchunguzi (“wafichuaji”) dhidi ya ulipizaji kisasasi. Kwa hivyo, IOM imepitisha Sera ya Ulinzi dhidi ya Ulipizaji Kisasi kwa kuripoti mienendo mibaya au kushirikiana na uchunguzi na ukaguzi.
Kwa madhununi ya Sera ya Ulipizaji Kisasi ya IOM, ulipizaji kisasi unamaanisha hatua yoyote ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja yenye madhara kuhusu ajira au mazingira ya kazi ya wafanyakazi wa IOM. Lazima iwe hatua hii ilipendekezwa, kutishiwa au kuchukuliwa dhidi ya wafanyakazi wa IOM kwa sababu walijihusisha na Shughuli Inayolindwa.
Inachukuliwa kuwa wafanyakazi wa IOM wameshiriki katika Shughuli Inayolindwa wakati:
- Wanaripoti tuhuma za mienendo mibaya, inayojumuisha unyanyasaji, unyanyasaji wa kijinsia, na matumizi mabaya ya mamlaka, kwa Ofisi ya Uangalizi wa Ndani (OIO) au kupitia kwa jukwaa la kuripoti mienendo mibaya la IOM, “We Are All In” (www.weareallin.iom.int);
- Wanaripoti mienendo mibaya, inayojumuisha unyanyasaji, unyanyasaji wa kijinsia, na matumizi mabaya ya mamlaka, kwa afisa ambaye ana mamlaka ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja ya usimamizi juu ya anayeripoti, ikiwa ni pamoja na msimamizi wa karibu au msimamizi mwingine anayefaa kama vile Afisa Mkuu wa IOM katika nchi au mkuu wa idara au ofisi inayohusika.
- Wanashirikiana kwa nia njema na ukaguzi au uchunguzi ulioidhinishwa ipasavyo.
Wafanyakazi wa IOM wanaojihusisha na Shughuli Inayolindwa kwa nia njema wana haki ya kulindwa dhidi ya ulipizaji kisasi.
- Mifano ya ulipizaji kisasi
-
- Msimamizi anamzuia kimakusudi mfanyakazi ambaye alimripoti kwa tuhuma za mienendo mibaya kupitia kwa jukwaa la kuripoti mienendo mibaya la “We Are All In” (www.weareallin.iom.int) asifanye kazi kwenye miradi muhimu.
- Meneja kimakusudi hamwajiri mfanyakazi aliyehitimu kwa nafasi mpya kutokana na mfanyakazi husika kuhojiwa na Ofisi ya Uangalizi wa Ndani (OIO) kama sehemu ya uchunguzi wa madai ya mienendo mibaya.
- Msimamizi anamwandikia mfanyakazi tathmini hasi ya utendaji isiyostahili kwa sababu aliripoti mienendo mibaya iliyoshukiwa katika kikundi chao, akisema kwamba yeye “hashirikiani na wenzake”.
- Taratibu za kushughulikia ulipizaji kisasi
-
Mchakato usio rasmi. IOM inahimiza utatuzi usio rasmi wa migogoro. Wafanyakazi wa IOM ambao wanaamini kwamba wametendewa vitendo vya kulipiza kisasi wanaweza kuchagua kutafuta suluhu isiyo rasmi ya hali hiyo kwa kuwasilisha suala hilo kwanza kwa msimamizi au meneja wa ngazi ya juu au Idara ya Usimamizi wa Rasilimali Watu (DHR). Watu binafsi wanaweza pia kutafuta usaidizi kutoka kwa Ofisi ya Mchunguza Kero (OOM).
Mchakato rasmi. Iwapo mchakato usio rasmi hautafaulu, au ikiwa wafanyakazi watachagua kutofuata mchakato usio rasmi, malalamiko rasmi ya ulipizaji kisasi yanapaswa kufanywa kwa maandishi kwa Ofisi ya Maadili na Mienendo (ECO) katika ECO@iom.int, au kwenye jukwaa la IOM la kuripoti mienendo mibaya, “We Are All In” (www.weareallin.iom.int).
- Hatua za ulinzi wa muda
-
Ofisi ya Maadili na Mienendo (ECO) inaweza, wakati wowote baada ya kupokea malalamiko ya ulipizaji kisasi, kupendekeza hatua za muda kwa mamlaka husika za IOM ili kumlinda mlalamikaji dhidi ya hatari ya ulipizaji kisasi au uwezekano wa ulipizaji kisasi. Hatua zinazopendekezwa zinaweza kujumuisha:
- Kutenganishwa kwa muda kwa mlalamikaji na anayedaiwa kuwa mlipizaji kisasi.
- Mabadiliko ya muda ya wakubwa unaoripoti kwao.
- Utambuaji wa kazi na/au kituo cha kazi mbadala kwa mlalamikaji au anayedaiwa kulipiza kisasi.
- Kuanzisha mipango ya kufanya kazi inayoweza kubadilika kwa ama mlalamikaji au anayedaiwa kulipiza kisasi.
- Kufikiria uwezekano wa likizo maalum yenye malipo kamili kwa mlalamikaji au anayedaiwa kulipiza kisasi.
- · Kusimamishwa kwa muda kwa utekelezaji wa kitendo kinachodaiwa cha kulipiza kisasi.
- Usalama na hali njema ya mlalamikaji
-
Ikiwa Ofisi ya Maadili na Mienendo (ECO) itagundua uwepo wa hatari ya moja kwa moja kwa usalama wa mlalamikaji, ECO itaarifu Ofisi ya Usalama wa Wafanyakazi ya IOM (OSS) au itamshauri mlalamikaji kutoa taarifa hiyo moja kwa moja kwa OSS.
Iwapo mlalamikaji ametoa taarifa ya kuhofia usalama wake, ECO itamshauri kuwasiliana na Afisa wa Ustawi wa Wafanyakzi (SWO).
- Hatua dhidi ya mlipizaji kisasi
-
Ulipizaji kisasi dhidi ya wafanyakazi wa IOM kwa sababu walishiriki katika Shughuli Zinazolindwa ni mwenendo usiotakiwa. Wafanyakazi wa IOM watakaopatikana wamejihusisha na ulipizaji kisasi watachukuliwa hatua za kinidhamu na hatua zingine zozote za kiutawala zinazofaa.
Wahudumu wasio wafanyakazi wa IOM na wafanyakazi wengine wanaweza kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria na masharti ya mkataba unaosimamia huduma zao na sera zingine zinazotumika kuhusu wahudumu wasio wafanyakazi. Hatua hizi zinaweza kujumuisha kusitishwa au kutosasisha mkataba bila notisi na kuwashataki kwa serikali za mitaa.
- Adhabu isiyo ya haki
-
Kwa kawaida, maneno ‘ulipizaji kisasi’ hutumiwa kurejelea hali anuwai ambapo mtu anahisi kuwa anaadhibiwa visivyo kwa sababu ya kitu ambacho amefanya.
Hata hivyo, Sera ya IOM ya Ulipizaji Kisasi inalenga kutoa ulinzi dhidi ya ulipizaji kisasi kwa wafichuaji wa IOM walio wafanyakazi wanaoshiriki katika Shughuli Zinazolindwa (yaani, kuripoti mienendo mibaya au kushirikiana na ukaguzi au uchunguzi).
Kitendo kibaya dhidi ya wafanyakazi wa IOM kutokana na sababu zingine mbali na kushiriki katika Shughuli Inayolindwa hakichukuliwi kuwa ulipizaji kisasi kwa mujibu wa Sera ya Ulipizaji Kisasi ya IOM. Kwa mfano, kitendo chochote hasi kinachopendekezwa, kutishiwa au kuchukuliwa dhidi ya wafanyakazi wa IOM kwa sababu ya kutokukubaliana au kumkosoa afisa wa ngazi ya juu hakitachukuliwa kuwa uipizaji kisasi. Hata hivyo, kinaweza kuchukuliwa kuwa matumizi mabaya ya mamlaka au udhalilishaji, ambazo ni aina zingine za mienendo mibaya.
Inaweza kuwa vigumu kutofautisha aina mbalimbali za mwenendo mbaya. Huhitaji kujua aina ya mwenendo mbaya ili uweze kuripoti. Iwapo utapata au kushuhudia mwenendo mbaya wowote, makosa au ikiwa unahisi kuwa kuna kosa lililofanyika, unapaswa kuripoti kwa Ofisi ya Uangalizi wa Ndani (OIO) ya IOM kupitia jukwaa la kuripoti mwenendo mbaya la IOM, “We Are All In” (www.weareallin.iom.int) au kwa baruapepe kwa oiointake@iom.int, hata kama huna hakika hiyo ni aina gani ya mwenendo mbaya.
Ilisasishwa mwisho: Machi 2024