IOM imejitolea kumaliza mienendo isiyofaa na dhuluma inayoendelezwa na wafanyakazi wa IOM dhidi ya wafanyakazi wenzao wa IOM, na imepitisha Sera ya Mazingira ya Kazi yenye Heshima ambayo inakataza i) ubaguzi; ii) udhalilishaji, unaojumuisha udhalilishaji wa kijinsia; na iii) matumizi mabaya ya mamlaka.

Udhalilishaji ni tabia yoyote isiyofaa au isiyokubalika inayofanywa na wafanyakazi wa IOM dhidi ya wafanyakazi wenzao wa IOM, iwe ya maneno au vitendo, ambayo inaweza kutarajiwa au kufikiriwa kuwa inakera au kufedhehesha. Udhalilishaji unaweza kuchukua sura ya maneno, ishara, au vitendo ambavyo vinatisha, kudhulumu, kutweza, kutenga, kudharau, kusababisha fedheha ya kibinafsi au aibu, wakati tabia kama hiyo inatatiza ufanyaji kazi au inaleta mazingira ya kazi ya kukera, yenye uhasama, au ya kutisha.

Udhalilishaji wa kijinsia ni tabia yoyote isiyokubalika yenye mwelekeo wa kijinsia inayofanywa na wafanyakazi wa IOM dhidi ya wafanyakazi wenzao wa IOM ambayo inaweza kutarajiwa au kufikiriwa kuwa inakera, au kufedhehesha; wakati tabia hiyo inatatiza ufanyaji kazi; inafanywa kuwa sharti la kuajiriwa; au wakati inaleta mazingira ya kazi ya kutisha, yenye uhasama, au ya kukera. Udhalilishaji wa kijinsia unaweza kutokea mahali pa kazi au kuhusiana na kazi kwa mfano, wakati wa kusafiri kwenda na kutoka kazini, saa za kazi au nje ya saa za kazi, wakati wa shughuli zinazohusiana na kazi (kama vile safari, mafunzo, matukio au shughuli za kijamii) na kupitia mawasiliano ya kielektroniki.

Udhalilishaji wa kijinsia haufai kuchanganywa na unyanyasaji na dhuluma za kijinsia (SEA), ambao umeelezwa katika ukurasa ufuatao https://weareallin.iom.int/sw/unyanyasaji-na-dhuluma-za-kijinsia.

Udhalilishaji na udhalilishaji wa kijinsia ni aina za Tabia za Dhuluma na ni mwenendo mbaya. Tabia za dhuluma pia hujumuisha (i) ubaguzi na (ii) matumizi mabaya ya mamlaka. Ubaguzi ni utendaji wowote usio wa haki au utofautishaji kiholela kwa misingi ya mbari, jinsi, mwelekeo wa kijinsia, jinsia, utambulisho, udhihirisho wa kijinsia, sifa za kijinsia, dini, utaifa, asili ya kabila, ulemavu, umri, lugha, asili ya kijamii, au sifa au hulka zingine zinazofanana za mtu. Matumizi mabaya ya mamlaka ni matumizi yasiyofaa ya nafasi ya ushawishi, uwezo au mamlaka dhidi ya mtu mwingine, kama vile kazi au masharti ya ajira. Matumizi mabaya ya mamlaka yanaweza pia kujumuisha tabia ambayo inasababisha mazingira ya kazi yenye uhasama au yanayokera na hujumuisha, ingawa hayajikiti tu katika, matumizi ya kutia woga, vitisho, usaliti, au ushurutishaji.

Mifano ya visa vya Tabia za Kidhuluma katika IOM ambavyo vilisababisha hatua za kinidhamu kuchukuliwa
  • Mfanyakazi alitoa kauli zisizofaa na zisizo za heshima ikiwa ni pamoja na lugha yenye ubaguzi wa kimbari, kuhusu mfanyakazi mwingine;
  • Mfanyakazi alituma barua pepe inayohusu ngono, inayokera na yenye utovu wa heshima kwa msimamizi;
  • Mfanyakazi alitisha wafanyakazi wawili na kumzomea mmoja wao;
  • Mfanyakazi alimshambulia mfanyakazi mwenzake akiwa kazini katika majengo ya IOM;
  • Mfanyakazi alimdhalilisha kijinsia mfanyakazi mwenzake.
Tabia isiyofaa

Tabia isiyofaa ni tabia inayotekelezwa na wafanyakazi wa IOM dhidi ya wafanyakazi wenzao wa IOM ambayo haiwiani na kanuni za mazingira ya kufanyia kazi yenye heshima, lakini ambayo haiwezi kuzorota na kufikia tabia yenye dhuluma/upotovu. Hata hivyo, inaweza na bado inapaswa kushughulikiwa kupitia njia za usuluhishaji zisizo rasmi (tazama “Uingiliaji kati mapema na mchakato usio rasmi”, hapa chini).

Zaidi ya hayo, kuwepo kwa kutokubaliana, migogoro, tabia isiyofaa au isiyokubalika hakumaanishi kuwa tabia yenye dhuluma imetokea, ikiwa inaweza kuelezwa vyema.

Uingiliaji kati mapema na machakato usio rasmi

Mwanachama yeyote wa wafanyakazi wa IOM ambaye anaamini kuwa ameathiriwa na tabia isiyofaa au yenye dhuluma anahimizwa kutatua hali hiyo kwa njia isiyo rasmi. Si lazima wafanyakazi wa IOM wafuate mbinu zisizo rasmi, hata hivyo, zinawapa walioathiriwa fursa ya kutatua suala lolote linalowasumbua kwa njia wazi, nyofu, isiyo vitisho, isiyo ugomvi, kwa hiari, na kwa njia rahisi. Utumiaji wa mifumo isiyo rasmi ya utatuzi hauwazuii wafanyakazi wa IOM kuripoti rasmi baadaye kwa Ofisi ya Uangalizi wa Ndani (OIO)

Wafanyakazi wa IOM wanahimizwa kusuluhisha matatizo moja kwa moja inapowezekana na wafanye hivyo mapema iwezekanavyo. Watu walioathiriwa wanaweza, kwa hiari yao na ikiwa wanahisi salama kufanya hivyo, kuwaendea wanaodaiwa kuwa wakosaji kuhusu matukio yanayoweza kuwa ya tabia isiyofaa au ya dhuluma na kuomba tabia hiyo ikome.

Wafanyakazi wa IOM walio na majukumu ya usimamizi wanaweza kuingilia kati katika hali zinazodaiwa kuwa zisizofaa au za tabia ya dhuluma kuhusu wale wanaowasimamia. Watu walioathiriwa wanaweza kuzungumzia suala hili na wasimamizi wao au meneja wa ngazi ya juu ili kuwafahamisha kuhusu matukio yanayoweza kuwa ya tabia isiyofaa au yenye dhuluma kwa upande wa anayedaiwa kuwa mkosaji na kuomba usaidizi ili kukomesha tabia kama hiyo.

Wasimamizi wanaweza kumfahamisha anayedaiwa kuwa mkosaji ili kuzuia kutokea tena kwa tabia inayochukuliwa kuwa isiyofaa au ya dhuluma na kutatua suala hilo.

Watu walioathiriwa wanaweza kutaka na wanahimizwa kutafuta usaidizi usio rasmi kutoka kwa Ofisi ya Mchunguza Kero (OOM) na Mtandao wake wa Vitovu vya Mahali pa Kazi penye Heshima (RWFP).

Mchakato Rasmi

Iwapo mchakato usio rasmi hautafaulu au ikiwa wafanyakazi wa IOM watachagua kutoutumia, ripoti rasmi ya madai ya tabia yenye dhuluma inaweza kuwasilishwa kwa Ofisi ya Uangalizi wa Ndani (OIG) ya IOM. Hili linaweza kufanywa kupitia oiointake@iom.int, moja kwa moja kwa wafanyakazi wa uchunguzi wa OIO, au kupitia jukwaa la kuripoti tabia mbaya la IOM, “We Are All In” (www.weareallin.iom.int). Ripoti rasmi zilizopokelewa na ofisi zingine au watu zinastahili kutumwa kwa OIO mara moja na mpokeaji, bila usambazaji zaidi.

Ingawa wafanyakazi wa IOM wana jukumu la kuripoti tabia isiyofaa wanayojua imetokea, hata kama hawahusiki moja kwa moja, tabia za dhuluma kama zilivyoelezwa hapo juu zinastahili kuripotiwa kwa uangalifu na kwa kuzingatia chaguo linalopendelewa na mtu aliyeathiriwa. Wafanyakazi wa IOM wanaoripoti tabia isiyofaa kwa nia njema wana haki ya kulindwa dhidi ya ulipizaji kisasi. (tazama https://weareallin.iom.int/sw/ulipizaji-kisasi).

Ripoti rasmi zinaweza kutolewa bila mtoaji kujitambulisha. Kwa jumla, ripoti rasmi zinastahili kutolewa katika muda uliowekwa.

Hatua za Muda

Ukisubiri tathmini ya mwanzo, mchakato rasmi au mchakato unaofuata wa nidhamu, OIO na/au Ofisi ya Masuala ya Kisheria (LEG) inaweza kumtahadharisha Mkuu wa Utawala husika au Idara ya Usimamizi wa Rasilimali Watu (DHR) kwamba hatua za muda zinafaa kuzingatiwa. Huenda hili linahitajika, kwa mfano, ili kulinda uadilifu wa uchunguzi, kuzuia kutokea au kurudiwa kwa tabia yenye dhuluma inayoweza kutokea na/au kushhughulikia hatari za kulipiza kisasi. Hatua kama hizo zinaweza kujumuisha:

  • Kutenga mtuhumiwa na mtu aliyeathiriwa wasikutane;
  • Utambulisho wa majukumu mbadala kwa mtu aliyeathiriwa au mtuhumiwa;
  • Kuanzisha mipango ya kufanya kazi itakayomfaa ama mtuhumiwa au mtu aliyeathiriwa;
  • Kufikiria uwezekano wa kutoa likizo maalum yenye malipo kamili kwa ama mtuhumiwa au mtu aliyeathiriwa;
  • Mabadiliko ya muda ya utaratibu wa wadogo kuripoti kwa wakubwa kazini;
  • Kusimamishwa kazi kwa muda kwa mfanyakazi akiwa analipwa au bila malipo

 

Inaweza kuwa vigumu kutofautisha aina mbalimbali za mwenendo mbaya. Huhitaji kujua aina ya mwenendo mbaya ili uweze kuripoti. Iwapo utapata au kushuhudia mwenendo mbaya wowote, makosa au ikiwa unahisi kuwa kuna kosa lililofanyika, unapaswa kuripoti kwa Ofisi ya Uangalizi wa Ndani (OIO) ya IOM kupitia jukwaa la kuripoti mwenendo mbaya la IOM, “We Are All In” (www.weareallin.iom.int) au kwa baruapepe kwa oiointake@iom.int, hata kama huna hakika hiyo ni aina gani ya mwenendo mbaya.


Ilisasishwa mwisho: Machi 2024