Je, ninahitaji kujua kategoria ya mwenendo mbaya ili niweze kutuma ripoti?

Hapana. Ukikumbana na au kushuhudia mwenendo mbaya wowote, makosa au ukihisi kwamba kuna jambo baya, unapaswa kuripoti kwa Ofisi ya Uangalizi wa Ndani ya IOM (OIO) kupitia We Are All In (www.weareallin.iom.int) au kwa baruapepe kupitia oiointake@iom.int, hata kama huna hakika kuhusu kategoria ya mwenendo huo mbaya. OIO hupokea na kutathmini ripoti zote za mienendo mibaya, isipokuwa ripoti za ulipizaji kisasi ambazo hupokelewa na kutathminiwa na Ofisi ya maadili na Mienendo (ECO). Kama sehemu ya mchakato huu, OIO/ECO watabainisha aina ya mwenendo mbaya ulioripotiwa.

Ukitaka kujifunza zaidi kuhusu aina za mienendo mibaya, unaweza kutembelea kurasa husika katika www.weareallin.iom.int ambazo zinatoa taarifa zaidi kuhusu baadhi ya aina za mienendo mibaya ikiwa ni pamoja na, unyanyasaji na dhuluma za kijinsia na, ulaghai, ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali, udhalilishaji, unaojumuisha udhalilishaji wa kijinsia na ulipizaji kisasi.

Je, ninaweza kuripoti bila kufichua jina langu?

Ndiyo. Unaweza kuripoti bila kutaja jina lako. Jukwaa la kuripoti la “We Are All In” ni chombo ambacho kinatuma ripoti za siri, zilizosimbwa moja kwa moja hadi kwa Ofisi ya Uangalizi wa Ndani (OIG) ya IOM, isipokuwa ripoti za ulipizaji kisasi, ambazo hutumwa kwa Ofisi ya Maadili na Mienendo (ECO). Chombo hiki kilitengenezwa kikiwa na vipengele vya ulinzi ambavyo vinamwezesha mtu kuripoti madai kwa siri.

Si lazima utoe jina lako, lakini OIO (au ECO) watahitaji madai yaliyo wazi na mahususi ili kuendelea. Kwa mfano, katika ripoti kuhusu Unyanyasaji na Dhuluma za Kijinsia (SEA), lazima OIO wajue kilichotokea na wawe na maelezo ya kutosha ya kuwatambua waathiriwa na watuhumiwa wa uhalifu. Maelezo yanayohitajika na OIO (au ECO) ni tofauti katika kila kesi na ikiwa OIO (au ECO) hawawezi kuwasiliana nawe kwa maelezo zaidi, huenda wasiweze kutathmini ripoti yako kikamilifu, au kuendelea na uchunguzi, ikiwa itahitajika.

Nikimripoti mtu, atajua kwamba ni mimi niliyefanya hivyo?

IOM inajitahidi kuhakikisha kuwa jina lako linawekwa siri. Hata hivyo, wakati mwingine IOM inahitaji kufichua majina ya walalamikaji wakati wa mchakato wa uchunguzi. Lazima IOM ifuate taratibu zilizo sahihi na iheshimu haki za kila anayehusika, ambazo pia zinajumuisha haki za mtu anayetuhumiwa.

Lazima anayechunguzwa aweze kuona ushahidi na taarifa zinazotumiwa dhidi yake. Hii ina maana kwamba huenda anayetuhumiwa akapewa malalamiko hayo.

Pia, huenda IOM ikalazimika kufichua mlalamikaji ni nani ikiwa:

  • Mtuhumiwa anahitaji kumjua ili kuandaa utetezi wake
  • Jina lake linahitajika baadaye katika mchakato wa kiutawala, kinidhamu au kimahakama

Na hatimaye, kuna uwezekano kwamba maelezo kuhusu uchunguzi yanaweza kufichuliwa kwa sababu ambazo IOM haiwezi kudhibiti, kama vile hali ambapo wafanyakazi wanakiuka sheria za IOM na kujadili tukio licha ya kuombwa kuiweka taarifa hiyo siri.

Ikiwa nitawasilisha ripoti, nitapata jibu?

Ofisi ya Uangalizi wa Ndani (OIO) itakujulisha kwamba imepokea ripoti yako.

OIO pia inaweza:

  • Kukuuliza maswali
  • Kukuomba utoe taarifa ya ushahidi au uhojiwe kama shahidi

Ukiripoti ulipizaji kisasi, ripoti yako itatathminiwa na Ofisi ya Maadili an Mienendo (ECO), ambayo Itakujulisha kuwa imepokea ripoti yako na huenda ikakuomba utoe maelezo zaidi.

Je, uchunguzi ni wa siri

IOM hujitahidi kuhakikisha kwamba taarifa nyeti zinasalia kuwa za siri. Wale wanaohusika katika uchunguzi hawapaswi kujadili sehemu yoyote yake na mtu yeyote isipokuwa wachunguzi. Iwapo mfanyakazi wa IOM atashiriki taarifa za siri na mtu mwingine asiye mchunguzi, anaweza kuadhibiwa. Iwapo wafanyakazi wengine wa IOM (kama vile washauri) watashiriki taarifa za siri na mtu mwingine asiye mchunguzi, mkataba wao na IOM unaweza kusitishwa.

Usiri ni muhimu kwa sababu unalinda faragha ya watu, usalama na haki ya kufuatwa kwa utaratibu unaostahili. Pia husaidia kuweka ushahidi na mashahidi salama na hulinda uadilifu wa uchunguzi.

IOM itatoa taarifa za siri pale inapohitajika watu wajue ikiwa tu ni muhimu kwa uchunguzi au zinahitajika kwa ajili ya haki za kiutaratibu za watu wanaohusika, ikiwa ni pamoja na mhusika ambaye ni mlalamishi.

Inachukua muda gani kuchunguza kesi?

Muda wa uchunguzi hutegemea mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na:

  • Uchangamano na uzito wa kesi
  • Idadi ya wahusika na waathiriwa wanaohusika
  • Upatikanaji wa taarifa na ushahidi
  • Upatikanaji wa rasilimali
  • Idadi na umuhimu kiulinganishi wa kesi zingine zinazochunguzwa
Serikali za mitaa zinahusika vipi katika kesi ya IOM?

Wafanyakazi wa IOM hawapaswi kuripoti masuala yoyote kwa serikali za mitaa isipokuwa katika hali ya dharura/hatari inayoelekea kutokea na ya lazima, na baada ya hapo sharti suala hilo liripotiwe mara moja kwa Ofisi ya Masuala ya Kisheria (LEG) ya IOM kupitia leg@iom.int.

Vinginevyo, masuala ambayo yanafaa kupelekwa kwa serikali za mitaa yanapaswa kutumwa kwa LEG kwa uamuzi wa rufaa kama hiyo.

Kuwasilisha jambo kwa serikali za mitaa kunaweza pia kuhitaji idhini ya Mkurugenzi Mkuu kwa kuwa kunaweza kuhusisha kuondolewa kwa haki na kinga wanazotengewa.

Inakuwaje ikiwa ninaripoti mwenendo mbaya uliofanywa na mtu ambaye si mfanyakazi wa IOM?

Unapaswa kuripoti mwenendo mbaya uliofanywa na mtu yeyote anayefanya kazi na IOM, hata kama ameajiriwa na au anafanyia kazi mashirika mengine. Hawa watajumuisha:

  • Wafanyakazi wa IOM, washauri na wakufunzi
  • Wakandarasi wa IOM, wafanyakazi wao na wafanyakazi wengine
  • Mtu mwingine yeyote anayefanya kazi kwenye miradi ya IOM

Wasiwasi, tuhuma na/au madai ya mienendo mibaya yanapaswa kuripotiwa kwa Ofisi ya Uangalizi wa Ndani ya IOM (OIG) kupitia jukwaa la kuripoti la “We Are All In” (https://weareallin.iom.int) au kwa baruapepe kupitia oigintake@iom.int. Ikiwa mshukiwa wa uhalifu anafanya kazi katika shirika lingine la Umoja wa Mataifa, OIO wa IOM anaweza kupeleka kesi hiyo kwa ofisi ya uchunguzi ya shirika hilo.

Hifadhidata inayofuatilia matukio ya unyanyasaji na dhuluma za kijinsia (SEA) na udhalilishaji wa kijinsia (SH) ni nini? Clear Check ni nini?

Clear Check ni hifadhidata ya Umoja wa Mataifa inayotumiwa kukagua waomba kazi. Hifadhidata hiyo inajumuisha watu ambao ufanyaji kazi wao na shirika la mfumo wa Umoja wa Mataifa uliisha kwa sababu ya uamuzi kwamba walitekeleza udhalilishaji wa kijinsia (SH) au unyanyasaji na dhuluma za kijinsia (SEA). Pia inaruhusu ujumuishaji wa watu binafsi wenye madai yanayosubiri uamuzi ambao wanaondoka Umoja wa Mataifa kabla ya kukamilika kwa uchunguzi na/au mchakato wa kinidhamu. Lengo la Clear Check ni kuzuia kuajiriwa tena kwa watu hawa katika mfumo wa Umoja wa Mataifa. IOM imekubali kutumia zana hii.

Ikiwa tukio la mwenendo mbaya katika IOM linahitaji usajili katika mfumo wa Clear Check wa IOM, Idara ya Usimamizi wa Rasilimali Watu ya IOM itawajibikia usajili huo.